Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijijini vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wote, kwa wakati, uhakika na muda wote.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga wakati wa ziara iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia UCSAF ya kuwapeleka wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu za mkononi, hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na changamoto zilizopo kwa wananchi wa maeneo husika. Wakiwa kwenye ziara hiyo kata ya Jipe iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro Eng.

 Ulanga amesema kuwa mnara wa Vodacom uliojengwa kwenye eneo hilo unahudumia zaidi ya wananchi 1,200 kwenye vijiji zaidi ya nane. Hadi hivi sasa UCSAF imejenga minara ya simu za mkononi kwenye maeneo saba yaliyopo Wilaya ya Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi. Vile vile, Kamati imetembelea minara iliyopo kata ya Nkalamo iliyopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Eng. Ulanga ameongeza kuwa Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili ziweze kufikisha mawasiliano kwenye vijiji vyote nchi nzima ambapo hadi hivi sasa UCSAF imetoa jumla ya dola za marekani milioni 41.5 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 93.3 kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwenye kata 518 ambazo zitajengwa minara ya mawasiliano. Mpaka sasa jumla ya kata 391 kati ya kata 518 zimefikishiwa huduma ya mawasiliano katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwezi Machi 2013 mpaka mwezi Agosti 2017 mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alipofanya ziara ya mawasiliano vijijini kwenye Wilaya ya Bahi, Chamwino mkoani Dodoma na Gairo kwenye mkoa wa Morogoro, ameziagiza kampuni za simu kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano vijijini zinapatikana masaa yote 24, siku saba za wiki na katika kipindi cha mwaka mzima bila kukatika, kwa uhakika na kwa wakati wote. 

Hali ya ukosefu wa mawasiliano kwa nyakati za usiku imekuwa ikijitokeza kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini ambako hakuna nishati ya uhakika ya umeme ambapo kampuni za simu zinatumia umeme wa jua kuendesha minara ili iweze kutoa mawasiliano kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King (wa kwanza kulia) akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Kweinsewa kilichopo kata ya Nkolamo, wilaya ya Korogwe Vijijini mkoani Tanga wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa minara na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye vijiji.
Bibi Mwanafuraha Nyange, mkazi wa kijiji cha ziwa Jipe kilichopo Kata ya Jipe wilaya ya Mwanga kwenye mkoa wa Kilimanjaro akieleza umuhimu wa mawasiliano vijijini kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu na wakazi wa kijiji cha ziwa Jipe kilichopo wilayani Mwanga mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...